الإسراء
Al-Isra
Hati
Tafsiri
Gusa neno la Kiarabu ili kuona usomaji, muundo na mzizi wake.
بِسْمِ ٱللَّهِ ٱلرَّحْمَٰنِ ٱلرَّحِيمِ
- Ali Muhsin Al-BarwaniSUBHANA, Ametakasika aliye mchukua mja wake usiku mmoja kutoka Msikiti Mtukufu mpaka Msikiti wa Mbali, ambao tumevibariki vilivyo uzunguka, ili tumuonyeshe baadhi ya Ishara zetu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia na Mwenye kuona.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa tukampa Musa Kitabu, na tukakifanya uwongofu kwa Wana wa Israili. (Tukawambia): Msiwe na mtegemewa ila Mimi!
- Ali Muhsin Al-BarwaniEnyi kizazi tuliyo wachukua pamoja na Nuhu! Hakika yeye alikuwa mja mwenye shukrani.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa tukawahukumia Wana wa Israili katika Kitabu kwamba: Hakika nyinyi mtafanya fisadi katika nchi mara mbili, na kwa yakini mtapanda kiburi, kiburi kikubwa.
- Ali Muhsin Al-BarwaniBasi itapo fika ahadi ya kwanza yake tutakupelekeeni waja wetu wa kali kwa vita. Watakuingilieni ndani ya majumba. Na hii ilikuwa ahadi iliyo timizwa.
- Ali Muhsin Al-BarwaniKisha tukakurudishieni nguvu zenu dhidi yao, na tukakusaidieni kwa mali na wana, na tukakujaalieni mkawa wengi zaidi.
- Ali Muhsin Al-BarwaniBasi mkifanya wema, mnajifanyia wema nafsi zenu. Na mkifanya ubaya, mnajifanyia wenyewe. Na ikifika ahadi ya mwisho ili waziharibu nyuso zenu, na waingie Msikitini kama walivyo ingia mara ya kwanza, na waharibu kila walicho kiteka kwa uharibifu mkubwa.
- Ali Muhsin Al-BarwaniHuenda Mola wenu Mlezi akakurehemuni. Na mkirudia na Sisi tutarudia. Na tumeifanya Jahannamu kuwa ni gereza kwa ajili ya makafiri.
- Ali Muhsin Al-BarwaniHakika hii Qur'ani inaongoa kwenye ya yaliyo nyooka kabisa, na inawabashiria Waumini ambao wanatenda mema ya kwamba watapata malipo makubwa.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa yakwamba wale wasio iamini Akhera tumewaandalia adhabu chungu.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa mwanaadamu huomba shari kama vile aombavyo kheri, kwani mwanaadamu ni mwenye pupa.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa tumefanya usiku na mchana kuwa ishara mbili. Tena tukaifuta ishara ya usiku, na tukaifanya ishara ya mchana ni yenye mwangaza ili mtafute fadhila itokayo kwa Mola wenu Mlezi, na mpate kujua idadi ya miaka na hisabu. Na kila kitu tumekifafanua waziwazi.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa kila mtu tumemfungia a'mali yake shingoni mwake. Na Siku ya Kiyama tutamtolea kitabu atakacho kikuta kiwazi kimekunjuliwa.
- Ali Muhsin Al-BarwaniAtaambiwa: Soma kitabu chako! Nafsi yako inakutosha leo kukuhisabu.
- Ali Muhsin Al-BarwaniAnaye ongoka basi anaongoka kwa ajili ya nafsi yake. Na anaye potea basi anapotea kwa khasara yake mwenyewe. Wala habebi mbebaji mzigo wa mwengine. Wala Sisi hatuadhibu mpaka tumpeleke Mtume.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa pindi tukitaka kuuteketeza mji huwaamrisha wale wenye starehe na taanusi, lakini wao huendelea kutenda maovu humo. Basi hapo kauli huthibiti juu ya mji huo, nasi tukauangamiza kwa maangamizo makubwa.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa kaumu ngapi tumeziangamiza baada ya Nuhu! Na Mola wako Mlezi anatosha kabisa kuwa ni Mwenye kuzijua na kuziona dhambi za waja wake.
- Ali Muhsin Al-BarwaniAnaye taka yapitayo upesi upesi, tutafanya haraka kumletea hapa hapa tunayo yataka kwa tumtakaye. Kisha tumemwekea Jahannamu; ataingia humo hali ya kuwa ni mwenye kulaumiwa na kufurushwa.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa anaye itaka Akhera, na akazifanyia juhudi a'mali zake, naye ni Muumini, basi hao juhudi yao itakuwa ni ya kushukuriwa.
- Ali Muhsin Al-BarwaniWote hao tunawakunjulia - hawa na hao - katika neema za Mola wako Mlezi. Wala neema za Mola wako Mlezi hazizuiliki.
- Ali Muhsin Al-BarwaniAngalia vipi tulivyo wafadhili baadhi yao kuliko wenginewe. Na hakika Akhera ni yenye daraja kubwa zaidi na fadhila kubwa zaidi.
- Ali Muhsin Al-BarwaniUsimfanye mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu, usije ukawa wa kulaumiwa uliye tupika.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa Mola wako Mlezi ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema. Mmoja wao akifikia uzee, naye yuko kwako, au wote wawili, basi usimwambie hata: Ah! Wala usiwakemee. Na sema nao kwa msemo wa hishima.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa uwainamishie bawa la unyenyekevu kwa kuwaonea huruma. Na useme: Mola wangu Mlezi! Warehemu kama walivyo nilea utotoni.
- Ali Muhsin Al-BarwaniMola wenu anajua kabisa yaliyo nyoyoni mwenu. Ikiwa nyinyi mtakuwa wema, basi hakika Yeye ni Mwenye kuwaghufiria wanao tubia kwake.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa mpe aliye jamaa yako haki yake, na masikini, na msafiri; wala usitumie ovyo kwa fujo.
- Ali Muhsin Al-BarwaniHakika wabadhirifu ni ndugu wa Mashet'ani. Na Shet'ani ni mwenye kumkufuru Mola wake Mlezi.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa ikiwa unajikurupusha nao, nawe unatafuta rehema ya Mola wako Mlezi unayo itaraji, basi sema nao maneno laini.
- Ali Muhsin Al-BarwaniWala usiufanye mkono wako kama ulio fungwa shingoni mwako, wala usiukunjue wote kabisa, utabaki ukilaumiwa muflisi.
- Ali Muhsin Al-BarwaniHakika Mola wako Mlezi humkunjulia riziki amtakaye, na humpimia amtakaye. Hakika Yeye kwa waja wake ni Mwenye kuwajua na kuwaona.
- Ali Muhsin Al-BarwaniWala msiwauwe wana wenu kwa kuogopa umasikini. Sisi tunawaruzuku wao na nyinyi. Hakika kuwaua hao ni khatia kubwa.
- Ali Muhsin Al-BarwaniWala msikaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya.
- Ali Muhsin Al-BarwaniWala msiuwe nafsi ambayo Mwenyezi Mungu amekataza isipo kuwa kwa haki. Na aliye uliwa kwa kudhulumiwa basi tumempa madaraka mrithi wake. Lakini asipite mpaka katika kuuwa. Kwani yeye anasaidiwa.
- Ali Muhsin Al-BarwaniWala msiyakaribie mali ya yatima, isipo kuwa kwa njia iliyo bora, mpaka afike utuuzimani. Na timizeni ahadi. Kwa hakika ahadi itasailiwa.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa timizeni kipimo mpimapo. Na pimeni kwa mizani zilizo sawa. Hayo ni wema kwenu na khatimaye ndio bora.
- Ali Muhsin Al-BarwaniWala usiyafuate usiyo na ujuzi nayo. Hakika masikio, na macho, na moyo - hivyo vyote vitasailiwa.
- Ali Muhsin Al-BarwaniWala usitembee katika ardhi kwa maringo. Hakika wewe huwezi kuipasua ardhi wala kufikia urefu wa milima.
- Ali Muhsin Al-BarwaniHaya yote ubaya wake ni wenye kuchukiza kwa Mola wako Mlezi.
- Ali Muhsin Al-BarwaniHaya ni katika hikima alizo kufunulia Mola wako Mlezi. Wala usimweke pamoja na Mwenyezi Mungu mungu mwengine, usije ukatupwa katika Jahannamu ukilaumiwa na kufurushwa.
- Ali Muhsin Al-BarwaniJe! Mola wenu Mlezi amekuteulieni wavulana, na Yeye akawafanya Malaika ni banati zake? Kwa hakika nyinyi mnasema usemi mkubwa.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa tumekwisha bainisha katika Qur'ani hii ili wapate kukumbuka. Lakini haikuwazidisha ila kuwa mbali nayo.
- Ali Muhsin Al-BarwaniSema: Lau kuwa wangeli kuwa pamoja naye miungu mingine kama wasemavyo, basi wangeli tafuta njia ya kumfikia Mwenye Kiti cha Enzi.
- Ali Muhsin Al-BarwaniSubhanahu Wa Taa'la, Ametakasika na Ametukuka juu kabisa na hayo wanayo yasema.
- Ali Muhsin Al-BarwaniZinamtakasa zote mbingu saba na ardhi na vyote viliomo ndani yake. Na hapana kitu ila kinamtakasa kwa sifa zake. Lakini nyinyi hamfahamu kutakasa kwake. Hakika Yeye ni Mpole na Mwenye maghfira.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa unapo soma Qur'ani tunaweka baina yako na wale wasio iamini Akhera pazia linalo wafunika.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa tunaweka vifuniko juu ya nyoyo zao wasije wakaifahamu, na tunaweka kwenye masikio yao uziwi. Na unapo mtaja katika Qur'ani Mola wako Mlezi peke yake, basi wao hugeuka nyuma wakenda zao.
- Ali Muhsin Al-BarwaniSisi tunajua vyema kabisa sababu wanayo sikilizia wanapo kusikiliza, na wanapo nong'ona. Wanapo sema hao madhaalimu: Nyinyi hamumfuati isipo kuwa mtu aliye rogwa.
- Ali Muhsin Al-BarwaniTazama vipi wanavyo kupigia mifano. Basi wamepotea. Kwa hivyo hawawezi kuipata njia.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa walisema: Je! Tutapo kuwa mifupa na mapande yaliyo vurugika, tutafufuliwa kwa umbo jipya?
- Ali Muhsin Al-BarwaniSema: Kuweni hata mawe na chuma.
- Ali Muhsin Al-BarwaniAu umbo lolote mnalo liona kubwa katika vifua vyenu. Watasema: Nani atakaye turudisha tena? Sema: Yule yule aliye kuumbeni mara ya kwanza! Watakutikisia vichwa vyao, na watasema: Lini hayo? Sema: A'saa yakawa karibu!
- Ali Muhsin Al-BarwaniSiku atakapo kuiteni, na nyinyi mkamuitikia kwa kumshukuru, na mkadhani kuwa hamkukaa ila muda mdogo tu.
- Ali Muhsin Al-BarwaniWaambie waja wangu waseme maneno mazuri, maana Shet'ani huchochea ugomvi baina yao. Hakika Shet'ani ni adui aliye dhaahiri kwa mwanaadamu.
- Ali Muhsin Al-BarwaniMola wenu Mlezi anakujueni vilivyo. Akipenda atakurehemuni, na akipenda atakuadhibuni. Na hatukukutuma ili uwe mlinzi juu yao.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa Mola wako Mlezi anawajua vilivyo waliomo mbinguni na katika ardhi. Na hakika tumewafadhilisha baadhi ya Manabii kuliko wengine; na Daudi tulimpa Zaburi.
- Ali Muhsin Al-BarwaniSema: Waombeni hao mnao wadaia badala yake Yeye. Hawawezi kukuondoleeni madhara, wala kuyaweka pengine.
- Ali Muhsin Al-BarwaniHao wanao waomba, wao wenyewe wanatafuta njia ya kwendea kwa Mola wao Mlezi - hata miongoni mwao walio karibu mno - na wanataraji rehema zake na wanaikhofu adhabu yake. Hakika adhabu ya Mola wako Mlezi yafaa kutahadhari nayo.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa hapana mji wowote ila Sisi tutauteketeza kabla ya Siku ya Kiyama, au tutaupa adhabu kali. Haya yamekwisha andikwa katika Kitabu.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa hapana kinacho tuzuia kupeleka miujiza ila ni kuwa watu wa zamani waliikanusha. Na tuliwapa Wathamudi ngamia jike kuwa ni Ishara iliyo dhaahiri, lakini walidhulumu kwaye. Nasi hatupeleki Ishara ila kwa ajili ya kuhadharisha.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa tulipo kwambia: Hakika Mola wako Mlezi amekwisha wazunguka hao watu. Na hatukuifanya ndoto tulio kuonyesha ila ni kuwajaribu watu, na mti ulio laaniwa katika Qur'ani. Na tunawahadharisha, lakini haiwazidishii ila uasi mkubwa.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa pale tulipo waambia Malaika: Msujudieni Adam. Wakamsujudia isipo kuwa Iblisi. Akasema: Je! Nimsujudie uliye muumba kwa udongo?
- Ali Muhsin Al-BarwaniAkasema: Hebu nambie khabari ya huyu uliye mtukuza juu yangu. Ukiniakhirisha mpaka Siku ya Kiyama, hapana shaka nitawaangamiza dhuriya zake wasipo kuwa wachache tu.
- Ali Muhsin Al-BarwaniAkasema Mwenyezi Mungu: Ondokelea mbali! Atakaye kufuata katika wao, basi Jahannamu itakuwa ndiyo malipo yenu, malipo ya kutimia.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa wachochee uwawezao katika wao kwa sauti yako, na wakusanyie jeshi lako la wapandao farasi na waendao kwa miguu. Na shirikiana nao katika mali na wana, na waahidi. Na Shet'ani hawapi ahadi ila ya udanganyifu.
- Ali Muhsin Al-BarwaniHakika wewe huna mamlaka juu ya waja wangu. Na Mola wako Mlezi anatosha kuwa ni wa kutegemewa.
- Ali Muhsin Al-BarwaniMola wenu Mlezi ndiye anaye kuendesheeni marikebu katika bahari ili mtafute katika fadhila zake. Hakika Yeye ni Mwenye kukurehemuni nyinyi.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa inapo kufikieni taabu katika bahari, hao mnao waomba wanapotea, isipo kuwa Yeye tu. Na anapo kuvueni mkafika nchi kavu, mnageuka. Ama mwanaadamu ni mwingi wa kukanusha.
- Ali Muhsin Al-BarwaniJe! Mmeaminisha ya kuwa hatakudidimizeni upande wowote katika nchi kavu, au kwamba hatakuleteeni tufani la kokoto? Kisha msipate wa kumtegemea.
- Ali Muhsin Al-BarwaniAu mmeaminisha ya kuwa hatakurudisheni humo mara nyengine na kukupelekeeni kimbunga cha upepo akakuzamisheni kwa mlivyo kufuru, na kisha msipate wa kukunusuruni nasi.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa hakika tumewatukuza wanaadamu, na tumewapa vya kupanda nchi kavu na baharini, na tumewaruzuku vitu vizuri vizuri, na tumewafadhilisha kwa fadhila kubwa kuliko wengi miongoni mwa tulio waumba.
- Ali Muhsin Al-BarwaniSiku tutapo waita kila kikundi cha watu kwa mujibu wa wakifuatacho - basi atakaye pewa kitabu chake kwa mkono wake wa kulia, basi hao watasoma kitabu chao wala hawatadhulumiwa hata chembe.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa aliye kuwa hapa kipofu, basi atakuwa kipofu Akhera, na atakuwa aliye ipotea zaidi Njia.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa hakika walikaribia kukushawishi uache tuliyo kufunulia ili utuzulie mengineyo. Na hapo ndio wangeli kufanya rafiki.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa lau kuwa hatukukuweka imara ungeli karibia kuwaelekea kidogo.
- Ali Muhsin Al-BarwaniHapo basi bila ya shaka tungeli kuonjesha adhabu mardufu ya uhai, na adhabu mardufu ya kifo. Kisha usinge pata mtu wa kukunusuru nasi.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa walitaka kukukera ili uitoke nchi. Na hapo wao wasingeli bakia humo ila kwa muda mchache tu.
- Ali Muhsin Al-BarwaniHuo ndio mwendo kwa Mitume tulio watuma kabla yako. Wala hupati mabadiliko katika mwendo wetu.
- Ali Muhsin Al-BarwaniShika Sala jua linapo pinduka mpaka giza la usiku, na Qur'ani ya al fajiri. Hakika Qur'ani ya alfajiri inashuhudiwa daima.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa amka usiku kwa ibada; ni ziada ya sunna khasa kwako wewe. Huenda Mola wako Mlezi akakunyanyua cheo kinacho sifika.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa sema: Mola wangu Mlezi! Niingize muingizo mwema, na unitoe kutoka kwema. Na unipe nguvu zinazo toka kwako zinisaidie.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa sema: Kweli imefika, na uwongo umetoweka. Hakika uwongo lazima utoweke!
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa tunateremsha katika Qur'ani yaliyo ni matibabu na rehema kwa Waumini. Wala hayawazidishii madhaalimu ila khasara.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa mwanaadamu tunapo mneemesha hugeuka na kujitenga kando. Na inapo mgusa shari hukata tamaa.
- Ali Muhsin Al-BarwaniSema: Kila mmoja anafanya kwa namna yake. Na Mola wenu Mlezi anajua aliye ongoka katika njia.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa wanakuuliza khabari za Roho. Sema: Roho ni katika mambo ya Mola wangu Mlezi. Nanyi hamkupewa katika ilimu ila kidogo tu.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa tungeli penda tungeli yaondoa tuliyo kufunulia. Kisha usingeli pata mwakilishi wa kukupigania kwetu kwa haya.
- Ali Muhsin Al-BarwaniIsipo kuwa iwe rehema itokayo kwa Mola wako Mlezi. Hakika fadhila yake kwako ni kubwa.
- Ali Muhsin Al-BarwaniSema: Wangeli kusanyika watu na majini ili walete mfano wa hii Qur'ani basi hawaleti mfano wake, hata wakisaidiana wao kwa wao.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa hakika tumewaeleza watu katika hii Qur'ani kwa kila mfano. Lakini watu wengi wanakataa isipo kuwa kukanusha tu.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa walisema: Hatutakuamini mpaka ututimbulie chemchem katika ardhi hii.
- Ali Muhsin Al-BarwaniAu uwe na kitalu cha mitende na mizabibu, na utupitishie mito kati yake ikimiminika.
- Ali Muhsin Al-BarwaniAu utuangushie mbingu vipande vipande kama ulivyo dai; au utuletee Mwenyezi Mungu na Malaika uso kwa uso.
- Ali Muhsin Al-BarwaniAu uwe na nyumba ya dhahabu, au upae mbinguni. Wala hatutaamini kupaa kwako mpaka ututeremshie kitabu tukisome. Sema: Subhana Rabbi, Ametakasika Mola wangu Mlezi! Kwani mimi ni nani isipo kuwa ni mwanaadamu na Mtume?
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa nini kilicho wazuilia watu kuamini ulipo wajia uwongofu isipo kuwa walisema: Je! Mwenyezi Mungu humtuma mwanaadamu kuwa ni Mtume?
- Ali Muhsin Al-BarwaniSema: Ingeli kuwa duniani wapo Malaika wanatembea kwa utulivu wao, basi bila ya shaka tungeli wateremshia Malaika kuwa ni Mtume wao.
- Ali Muhsin Al-BarwaniSema: Mwenyezi Mungu anatosha kuwa Shahidi baina yangu na nyinyi. Hakika Yeye anawajua vyema waja wake na anawaona.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa anaye mhidi Mwenyezi Mungu basi huyo ndiye aliye hidika. Na anaye wapotoa basi huto wapatia walinzi badala yake. Na tutawakusanya Siku ya Kiyama hali wakikokotwa juu ya nyuso zao, nao ni vipofu na mabubu na viziwi. Na makaazi yao ni Jahannamu. Kila moto ukifanya kusinzia tutazidi kuuchochea uwake kwa nguvu.
- Ali Muhsin Al-BarwaniHayo ni malipo yao kwa sababu walizikataa ishara zetu, na wakasema: Hivyo tukisha kuwa mifupa na mapande yaliyo vurugika tutafufuliwa kwa umbo jipya?
- Ali Muhsin Al-BarwaniKwani hawakuona ya kwamba Mwenyezi Mungu aliye umba mbingu na ardhi ni Mwenye kuweza kuumba mfano wao? Na Yeye amewawekea muda usio na shaka yoyote. Lakini madhaalimu hawataki ila ukafiri.
- Ali Muhsin Al-BarwaniSema: Lau kuwa nyinyi mnazimiliki khazina za rehema za Mola wangu Mlezi, basi hapana shaka mngeli zuia kuzitumia kwa ajili ya kukhofu. Na mwanaadamu tangu hapo tabia yake ni mchoyo!
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa kwa yakini tulimpa Musa ishara tisa zilizo wazi. Waulize Wana wa Israili alipo wafikia, na Firauni akawaambia: Hakika mimi nakuona wewe Musa umerogwa!
- Ali Muhsin Al-BarwaniMusa akasema: Wewe unajua bila ya shaka kuwa haya hakuyateremsha ila Mola Mlezi wa mbingu na ardhi ili kuwa ni ushahidi wa kuonekana. Na hakika mimi bila ya shaka nakuona wewe, Firauni, kuwa umekwisha angamia.
- Ali Muhsin Al-BarwaniBasi Firauni akataka kuwafukuza katika nchi. Kwa hivyo tukamzamisha yeye na walio kuwa pamoja naye wote.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa tukawaambia baada yake Wana wa Israili: Kaeni katika nchi. Itapo kuja ahadi ya Akhera tutakuleteni nyote pamoja.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa kwa Haki tumeiteremsha, na kwa Haki imeteremka. Na hatukukutuma ila uwe mbashiri na mwonyaji.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa Qur'ani tumeigawanya sehemu mbali mbali ili uwasomee watu kwa kituo, na tumeiteremsha kidogo kidogo.
- Ali Muhsin Al-BarwaniSema: Iaminini au msiiamini. Hakika wale walio pewa ilimu kabla yake, wanapo somewa hii, huanguka kifudifudi wanasujudu.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa wanasema: Subhana Rabbina, Ametakasika Mola wetu Mlezi! Hakika ahadi ya Mola wetu Mlezi lazima itimizwe!
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa huanguka kifudifudi na huku wanalia, na inawazidisha unyenyekevu.
- Ali Muhsin Al-BarwaniSema: Mwombeni Allah (Mwenyezi Mungu), au mwombeni Rahman (Mwingi wa Rehema), kwa jina lolote mnalo mwita. Kwani Yeye ana majina mazuri mazuri. Wala usitangaze Sala yako kwa sauti kubwa, wala usiifiche kwa sauti ndogo, bali shika njia ya kati na kati ya hizo.
- Ali Muhsin Al-BarwaniNa sema: Alhamdulillah, Himdi zote ni za Mwenyezi Mungu ambaye hana mwana, wala hana mshirika katika ufalme, wala hana rafiki wa kumsaidia kwa sababu ya udhaifu wake. Na mtukuze kwa utukufu mkubwa.