فصلت

Fussilat

Sura ya 41 · ya Makka · aya 54 · Mpangilio wa kuteremshwa: 61

Hati
Tafsiri

Gusa neno la Kiarabu ili kuona usomaji, muundo na mzizi wake.

بِسْمِ ٱللَّهِ ٱلرَّحْمَٰنِ ٱلرَّحِيمِ
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniH'a Mim
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniUteremsho huu umetoka kwa Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniHichi ni Kitabu kilicho pambanuliwa Aya zake, cha kusomwa kwa Kiarabu kwa watu wanao jua.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniKitoacho khabari njema, na chenye kuonya. Lakini wengi katika wao wamepuuza; kwa hivyo hawasikii.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa wakasema: Nyoyo zetu zimo katika vifuniko kwa hayo unayo tuitia, na masikio yetu yana uziwi, na baina yetu na wewe lipo pazia. Basi wewe tenda, nasi tunatenda.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniSema: Hakika mimi ni mtu kama nyinyi; inafunuliwa kwangu ya kwamba Mungu wenu ni Mungu Mmoja tu. Basi nyookeni sawa kumwendea Yeye, na mumtake msamaha, na ole wao wanao mshirikisha,
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniAmbao hawatoi Zaka na wanaikataa Akhera.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniHakika wanao amini na wakatenda mema watakuwa na ujira usio na ukomo.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniSema: Hivyo nyinyi mnamkataa aliye umba ardhi katika siku mbili, na mnamfanyia washirika? Huyu ndiye Mola Mlezi wa walimwengu wote.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa akaweka humo milima juu yake, na akabarikia humo na akakadiria humo chakula chake katika siku nne. Haya ni sawa kabisa kwa wanao uliza.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniKisha akazielekea mbingu, na zilikuwa moshi, akaziambia hizo na ardhi: Njooni, kwa khiari au kwa nguvu! Vyote viwili vikasema: Tumekuja nasi ni wat'iifu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniBasi akazifanya mbingu saba kwa siku mbili, na akazipangia kila mbingu mambo yake. Na tukaipamba mbingu ya chini kwa mataa na kwa ulinzi. Hichi ndicho kipimo cha Mwenyezi Mungu Mwenye Kujua.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniBasi wakipuuza wewe sema: Nakuhadharisheni adhabu mfano wa adhabu ya A'di na Thamudi,
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniWalipo wajia Mitume mbele yao na nyuma yao wakawaambia: Msimuabudu ila Mwenyezi Mungu! Wakasema: Angeli taka Mola wetu Mlezi bila ya shaka angeli wateremsha Malaika. Basi sisi hakika tunayakataa hayo mliyo tumwa.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniAma kina A'di walijivuna katika nchi bila ya haki, na wakasema: Nani aliye kuwa na nguvu kushinda sisi? Kwani wao hawakuona kwamba Mwenyezi Mungu aliye waumba ni Mwenye nguvu kushinda wao? Na wao wakawa wanazikataa Ishara zetu!
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniBasi tuliwapelekea upepo wa kimbunga katika siku za ukorofi, ili tuwaonjeshe adhabu ya kuwahizi katika uhai wa duniani, na bila ya shaka adhabu ya Akhera ina hizaya zaidi, na wala wao hawatanusuriwa.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa ama Thamudi tuliwaongoza, lakini walipenda upofu kuliko uwongofu. Basi uliwachukua moto wa adhabu ya kuwafedhehi kwa sababu ya yale waliyo kuwa wakiyachuma.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa tukawaokoa walio amini na wakawa wanamcha-mngu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa siku watakapo kusanywa maadui wa Mwenyezi Mungu kwenye Moto, nao wakikgawanywa kwa makundi.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniHata watakapo ufikia Moto yatawashuhudia masikio yao, na macho yao na ngozi zao kwa waliyo kuwa wakiyatenda.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa wao wataziambia ngozi zao: Kwa nini mmetushuhudilia? Nazo zitasema: Ametutamkisha Mwenyezi Mungu ambaye ametamkisha kila kitu! Na Yeye ndiye aliye kuumbeni mara ya kwanza, na kwake Yeye tu mtarejeshwa.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa hamkuwa wenye kujificha hata masikio yenu, na macho yenu, na ngozi zenu, zisikushuhudilieni. Lakini mlidhani kwamba Mwenyezi Mungu hayajui mengi katika mliyo kuwa mkiyatenda.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniBasi hiyo dhana yenu mliyo kuwa mkimdhania Mola wenu Mlezi. Imekuangamizeni; na mmekuwa miongoni mwa walio khasiri.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniBasi wakisubiri Moto ndio maskani yao. Na wakiomba radhi hawakubaliwi.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa tukawawekea marafiki, na wakawapambia yaliyo mbele yao na nyuma yao. Basi ikawathibitikia kauli wawe pamoja na mataifa yaliyo pita kabla yao, miongoni mwa majini na watu. Hakika hao wamekuwa ni wenye kukhasirika.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa walio kufuru walisema: Msiisikilize Qur'ani hii, na timueni zogo, huenda mkashinda.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniBasi hapana shaka tutawaonjesha hao walio kufuru adhabu kali, na hapana shaka tutawalipa malipo mabaya ya yale waliyo kuwa wakiyafanya.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniHayo ndiyo malipo ya Maadui wa Mwenyezi Mungu - Moto! Humo watakuwa na maskani ya kudumu, ndiyo malipo yao kwa sababu walikuwa wakizikataa Ishara zetu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa walio kufuru watasema: Mola wetu Mlezi! Tuonyeshe walio tupoteza miongoni mwa majini na watu ili tuwaweke chini ya miguu yetu, wapate kuwa miongoni wa walio chini kabisa.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniHakika walio sema: Mola wetu Mlezi ni Mwenyezi Mungu! Kisha wakanyooka sawa, hao huwateremkia Malaika wakawaambia: Msiogope, wala msihuzunike; nanyi furahini kwa Pepo mliyo kuwa mkiahidiwa.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniSisi ni vipenzi vyenu katika maisha ya dunia na katika Akhera, na humo mtapata kinacho tamaniwa na nafsi zenu, na humo mtapata mtakavyo vitaka.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNi takrima itokayo kwa Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa ni nani mbora wa kusema kuliko aitaye kwa Mwenyezi Mungu na akatenda mema, na akasema: Hakika mimi ni katika Waislamu?
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniMema na maovu hayalingani. Pinga uovu kwa lilio jema zaidi. Hapo yule ambaye baina yako naye pana uadui atakuwa kama rafiki jamaa wa kukuonea uchungu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniLakini hawapewi wema huu ila wanao subiri, wala hawapewi ila wenye bahati kubwa.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa Shet'ani akikuchochea kwa uchochezi wewe jikinge kwa Mwenyezi Mungu. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kujua.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa katika Ishara zake ni usiku na mchana, na jua na mwezi. Basi msilisujudie jua wala mwezi, bali msujudieni Mwenyezi Mungu aliye viumba, ikiwa nyinyi mnamuabudu Yeye tu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa ikiwa watajivuna, basi hao walioko kwa Mola wako Mlezi wanamtakasa Yeye usiku na mchana, na wao hawachoki.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa katika Ishara zake ni kwamba unaiona ardhi nyonge, lakini tunapo iteremshia maji mara unaiona inataharaki na kuumuka. Bila ya shaka aliye ihuisha ardhi ndiye atakaye huisha wafu. Hakika Yeye ni Muweza wa kila kitu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniHakika wale wanao upotoa ukweli uliomo katika Ishara zetu hawatufichikii Sisi. Je! Atakaye tupwa Motoni ni bora au atakaye kuja kwa amani Siku ya Kiyama? Tendeni mpendavyo, kwa hakika Yeye anayaona mnayo yatenda.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniKwa hakika wanayo yakataa mawaidha haya yanapo wajia (wataangamia), na haya bila ya shaka ni Kitabu chenye nguvu na utukufu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniHautakifikia upotovu mbele yake wala nyuma yake. Kimeteremshwa na Mwenye hikima, Msifiwa.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniHuambiwi ila yale yale waliyo ambiwa Mitume wa kabla yako. Hakika Mola wako Mlezi bila ya shaka ni Mwenye maghfira, na ni Mwenye adhabu chungu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa lau tungeli ifanya Qur'ani kwa lugha ya kigeni wangeli sema: Kwanini Aya zake haziku pambanuliwa? Yawaje lugha ya kigeni na Mtume Mwaarabu? Sema: Hii Qur'ani ni uwongofu na poza kwa wenye kuamini. Na wasio amini umo uziwi katika masikio yao, nayo kwao imezibwa hawaioni. Hao wanaitwa nao wako pahala mbali.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa hakika tulimpa Musa Kitabu, lakini pakatokea khitilafu kati yake. Na lau kuwa halikwisha tangulia neno la Mola wako Mlezi wangeli hukumiwa. Na hakika wao wamo katika shaka yenye kuwatia wasiwasi.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniAnaye tenda mema basi anajitendea mwenyewe nafsi yake, na mwenye kutenda uovu basi ni juu ya nafsi yake vile vile; wala Mola wako Mlezi si mwenye kuwadhulumu waja.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniUJUZI wa kuijua Saa ya Kiyama unarudishwa kwake tu Mwenyezi Mungu. Na matunda hayatoki katika mafumba yake, wala mwanamke hachukui mimba, wala hazai, ila kwa kujua kwake. Na siku atakayo waita, akawaambia: Wako wapi washirika wangu? Hapo watasema: Tunakiri kwako ya kwamba hapana miongoni mwetu anaye shuhudia hayo.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa wakawapotea wale walio kuwa wakiwaomba hapo kwanza, na wakawa na yakini kuwa hawana pa kukimbilia.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniMwanaadamu hachoki kuomba dua za kheri, na inapo mpata shari, mara huvunjika moyo akakata tamaa.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa pindi tukimwonjesha rehema itokayo kwetu baada ya kumgusa dhara, bila ya shaka husema: Haya nayastahiki mimi, wala sidhani kuwa Kiyama kitakuja. Na hata nikirudishwa kwa Mola wangu Mlezi bila ya shaka nina mema yangu kwake! Basi kwa yakini tutawaelezea walio kufuru hayo waliyo yatenda, na kwa yakini tutawaonjesha adhabu ngumu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa tukimneemesha mwanaadamu hugeuka na kujitenga upande, na inapo mgusa shari, huwa na madua marefu marefu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniSema: Mnaonaje! Ikiwa haya yanatoka kwa Mwenyezi Mungu, nanyi ikawa ndio mmeyakataa, ni nani aliye potea zaidi kuliko aliye katika upinzani wa mbali?
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniTutawaonyesha Ishara zetu katika upeo wa mbali na katika nafsi zao wenyewe mpaka iwabainikie kwamba haya ni kweli. Je! Haikutoshi kwamba Mola wako Mlezi kuwa Yeye ni Shahidi wa kila kitu?
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniAma wao wamo katika shaka ya kukutana na Mola wao Mlezi! Ama hakika Yeye amekizunguka kila kitu.