الأنبياء

Al-Anbya

Sura ya 21 · ya Makka · aya 112 · Mpangilio wa kuteremshwa: 73

Hati
Tafsiri

Gusa neno la Kiarabu ili kuona usomaji, muundo na mzizi wake.

بِسْمِ ٱللَّهِ ٱلرَّحْمَٰنِ ٱلرَّحِيمِ
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniIMEWAKARIBIA watu hisabu yao, nao wamo katika mghafala wanapuuza.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniHayawafikilii mawaidha mapya kutoka kwa Mola wao Mlezi ila huyasikiliza na huku wanafanya mchezo.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniZimeghafilika nyoyo zao. Na wale walio dhulumu hunong'onezana kwa siri: Ni nani ati huyu isipo kuwa ni binaadamu tu kama nyinyi! Mnauwendea uchawi hali nanyi mnaona?
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniAlisema: Mola wangu Mlezi anayajua yasemwayo mbinguni na katika ardhi. Na Yeye ni Mwenye kusikia Mwenye kujua.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniLakini wao walisema: Hizo ni ndoto za ovyo ovyo, bali amezizua tu, bali huyo ni mtunga mashairi. Basi atuletee miujiza kama walivyo tumwa wale wa mwanzo.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniHawakuamini kabla yao watu wa mji tulio uangamiza. Basi, je, wataamini hawa?
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa kabla yako hatukuwatuma ila watu wanaume tulio wapa wahyi (ufunuo). Basi waulizeni wenye ilimu ikiwa nyinyi hamjui.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniWala hatukuwafanya miili isiyo kula chakula, wala hawakuwa wenye kuishi milele.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniKisha tukawatimizia miadi, na tukawaokoa wao na tulio wataka, na tukawateketeza walio pita mipaka.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa hakika tumekuteremshieni Kitabu ambacho ndani yake yamo makumbusho yenu. Je! Hamzingatii?
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa mingapi katika miji iliyo kuwa ikidhulumu tumeiteketeza, na tukawasimamisha baada yao watu wengine.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniBasi walipo ihisi adhabu yetu, mara wakaanza kukimbia.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniMsikimbie! Na rejeeni kwenye zile zile starehe zenu, na maskani zenu, mpate kusailiwa!
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniWakasema: Ole wetu! Hakika sisi tulikuwa madhaalimu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniHakikuacha hicho kuwa kilio chao mpaka tukawafanya kama walio fyekwa, wamezimika.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyo baina yao kwa mchezo.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniKama tungeli taka kufanya mchezo tunge jifanyia Sisi wenyewe, lau kwamba tungeli kuwa ni wafanyao mchezo.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniBali tunaitupa kweli juu ya uwongo ikauvunja na mara ukatoweka. Na ole wenu kwa mnayo yazua.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa ni vyake Yeye tu Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na katika ardhi. Na walioko kwake hawafanyi kiburi wakaacha kumuabudu, wala hawachoki.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniWanamtakasa usiku na mchana, wala hawanyong'onyei.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniAu wamepata miungu katika ardhi inayo fufua?
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniLau wangeli kuwamo humo miungu wengine isipo kuwa Mwenyezi Mungu basi bila ya shaka hizo mbingu na ardhi zingeli fisidika. Subahana 'Llah Ametakasika Mwenyezi Mungu, Bwana wa A'rshi (Kiti cha Enzi), na hayo wanayo yazua.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniYeye hahojiwi kwa ayatendayo, na wao ndio wanao hojiwa kwa wayatendayo.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniAu wanawaabudu miungu mingine badala yake? Sema: Leteni ushahidi wenu! Haya ni ukumbusho wa hawa walio nami, na ukumbusho wa walio kabla yangu. Lakini wengi wao hawaijui kweli, na kwa hivyo wanapuuza.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa hatukumtuma kabla yako Mtume yeyote ila tulimfunulia ya kwamba hapana mungu isipo kuwa Mimi. Basi niabuduni Mimi tu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa wanasema: Arrahman, Mwingi wa Rehema, ana mwana! Subhanahu, Ametakasika na hayo! Bali hao (wanao waita wana) ni watumwa walio tukuzwa.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniHawamtangulii kwa neno, nao wanafanya amri zake.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniAnayajua yaliyo mbele yao na yaliyo nyuma yao. Wala hawamwombei yeyote ila yule anaye mridhia Yeye, nao kwa ajili ya kumwogopa wananyenyekea.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa yeyote kati yao atakaye sema: Mimi ni mungu, badala yake, basi huyo tutamlipa malipo yake Jahannamu. Hivyo ndivyo tuwalipavyo wenye kudhulumu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniJe! Hao walio kufuru hawakuona kwamba mbingu na ardhi zilikuwa zimeambatana, kisha Sisi tukazibabandua? Na tukajaalia kwa maji kila kilicho hai? Basi je, hawaamini?
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa tukaweka katika ardhi milima iliyo thibiti ili isiwayumbishe, na tukaweka humo njia pana ili wapate kuongoka.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa tukaifanya mbingu kuwa dari iliyo hifadhiwa, lakini wanazipuuza Ishara zake.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa Yeye ndiye aliye umba usiku na mchana na jua na mwezi, vyote katika anga vinaogelea.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNasi hatukumjaalia mwanaadamu yeyote kabla yako kuwa na maisha ya milele. Basi je! Ukifa wewe, wao wataishi milele?
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniKila nafsi itaonja mauti; na tunakujaribuni kwa mtihani wa shari na kheri. Na kwetu Sisi mtarejeshwa.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa wakikuona walio kufuru hawakufanyi wewe ila ni kitu cha maskhara tu, (wakisema): Je! Ndiye huyu anaye itaja miungu yenu? Na hali wao wanakataa kumkumbuka Arrahman, Mwingi wa Rehema!
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniMwanaadamu ameumbwa na haraka. Nitakuonyesheni Ishara zangu. Basi msinihimize.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa wanasema: Ahadi hii itatokea lini, ikiwa nyinyi mnasema kweli?
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniLau wangeli jua wale walio kufuru wakati ambao hawatauzuia Moto kwenye nyuso zao wala migongo yao, na wala hawatanusuriwa!
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniBali utawafikia kwa ghafla, na utawashitua na wala hawataweza kuurudisha, wala hawatapewa muhula!
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa Mitume walio kabla yako walikwisha dhihakiwa. Kwa hivyo wale walio wafanyia maskhara yaliwafika yale waliyo kuwa wakiyafanyia dhihaka.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniSema: Nani anaye kulindeni usiku na mchana na Arrahmani Mwingi wa Rehema? Bali wao wanapuuza kumkumbuka Mola wao Mlezi.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniAu wao wanao miungu watao weza kuwakinga nasi? Hao hawawezi kujinusuru nafsi zao, wala hawatalindwa nasi!
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniBali tuliwastarehesha hawa na baba zao mpaka umri ukawa mrefu kwao. Je, hawaoni ya kwamba Sisi tunaifikia ardhi tukiipunguza ncha zake? Basi je! Hao ni wenye kushinda?
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniSema: Mimi nakuonyeni kwa Wahyi. Na viziwi hawasikii wito wanapo onywa.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa wanapo guswa na mpulizo mmoja tu wa adhabu itokayo kwa Mola wako Mlezi, bila ya shaka wao husema: Ole wetu! Hakika tulikuwa wenye kudhulumu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNasi tutaweka mizani za uadilifu kwa Siku ya Kiyama. Basi nafsi haitadhulumiwa kitu chochote. Hata ikiwa ni uzito wa chembe ya khardali tutaileta. Nasi tunatosha kuwa washika hisabu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa kwa yakini tuliwapa Musa na Haaruni kipambanuzi, na mwangaza, na makumbusho kwa wachamngu,
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniAmbao wanamkhofu Mola wao Mlezi faraghani, na wanaiogopa Saa ya Kiyama.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa haya ni makumbusho yaliyo barikiwa, tuliyo yateremsha. Basi je! Mnayakataa?
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa hakika tulikwisha mpa Ibrahim uwongofu wake zamani, na tulikuwa tunamjua.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniAlipo mwambia baba yake na watu wake: Ni nini haya masanamu mnayo yashughulikia kuyaabudu?
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniWakasema: Tumewakuta baba zetu wakiyaabudu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniAkasema: Bila ya shaka nyinyi na baba zenu mmekuwa katika upotofu ulio dhaahiri.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniWakasema: Je! Umetujia kwa maneno ya kweli au wewe ni katika wachezao tu?
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniAkasema: Bali Mola wenu Mlezi ni Mola Mlezi wa mbingu na ardhi ambaye ndiye aliye ziumba. Na mimi ni katika wenye kuyashuhudia hayo.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa Wallahi! Nitayafanyia vitimbi masanamu yenu haya baada ya mkisha geuka kwenda zenu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniBasi akayavunja vipande vipande, ila kubwa lao, ili wao walirudie.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniWakasema: Nani aliye ifanyia haya miungu yetu? Hakika huyu ni katika walio dhulumu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniWakasema: Tumemsikia kijana mmoja akiwataja. Anaitwa Ibrahim.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniWakasema: Mleteni mbele ya macho ya watu, wapate kumshuhudia!
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniWakasema: Je! Wewe umeifanyia haya miungu yetu, ewe Ibrahim?
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniAkasema: Bali amefanya hayo huyu mkubwa wao. Basi waulizeni ikiwa wanaweza kutamka.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniBasi wakajirudi nafsi zao, wakasema: Hakika nyinyi mlikuwa madhaalimu!
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniKisha wakarejea kwenye ule ule upotovu wao wakasema: Wewe unajua kwamba hawa hawesemi.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniAkasema: Basi nyinyi mnawaabudu asiye kuwa Mwenyezi Mungu wasio kufaini kitu wala kukudhuruni?
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniAibu yenu nyinyi na hivyo mnavyo viabudu badala ya Mwenyezi Mungu! Basi nyinyi hamtii akilini?
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniWakasema: Mchomeni moto, na muinusuru miungu yenu, ikiwa nyinyi ni watendao jambo!
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniSisi tukasema: Ewe moto! Kuwa baridi na salama kwa Ibrahim!
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniWao walimkusudia maovu, lakini Sisi tukawafanya wao ndio walio khasiri.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa tukamwokoa yeye na Luut'i tukawapeleka kwenye nchi tulio ibariki kwa ajili ya walimwengu wote.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNaye tukampa Is-haq, na Yaaqub kuwa ni ziada. Na wote tukawajaalia wawe watu wema.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa tukawafanya maimamu wakiongoa watu kwa amri yetu. Na tukawafunulia watende kheri, na washike Sala, na watoe Zaka; na walikuwa wanatuabudu Sisi tu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa Luut'i tukampa hukumu na ilimu na tukamwokoa na ule mji ulio kuwa ukifanya maovu. Hakika hao walikuwa watu wabaya, wachafu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa tukamuingiza katika rehema yetu. Hakika yeye ni miongoni mwa watenda mema.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa Nuhu alipo ita zamani, nasi tukamuitikia, na tukamwokoa yeye na watu wake kutokana na shida kubwa.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa tukamnusuru na watu walio zikanusha Ishara zetu. Hakika hao walikuwa watu wabaya. Basi tukawazamisha wote.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa Daud na Suleiman walipo kata hukumu katika kadhiya ya konde walipo lisha humo mbuzi wa watu usiku. Na Sisi tulikuwa wenye kushuhudia hukumu yao hiyo.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniTukamfahamisha Suleiman. Na kila mmoja wao tulimpa hukumu na ilimu. Na tuliifanya milima na ndege kuwa pamoja na Daud imnyenyekee na imtakase Mwenyezi Mungu. Na Sisi ndio tulio fanya hayo.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa tukamfundisha kuunda mavazi ya vita kwa ajili yenu ili yakuhifadhini katika kupigana kwenu. Je! Mtakuwa wenye kushukuru?
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa tukamsahilishia Suleiman upepo wa kimbunga wendao kwa amri yake kwenye ardhi tuliyo ibarikia. Na Sisi ndio tunao jua kila kitu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa pia mashet'ani wanao mpigia mbizi na kufanya kazi nyenginezo. Na Sisi tulikuwa walinzi wao.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa Ayyubu, alipo mwita Mola wake Mlezi, akasema: Mimi yamenipata madhara. Na Wewe ndiye unaye rehemu kuliko wote wanao rehemu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniBasi tukamwitikia, na tukamwondolea madhara aliyo kuwa nayo, na tukampa watu wake na mfano wao pamoja nao kuwa ni rehema inayo toka kwetu, na ukumbusho kwa wafanyao ibada.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa Ismail, na Idris, na Dhulkifli - wote walikuwa miongoni mwa wanao subiri.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa tukawaingiza katika rehema yetu. Hakika wao walikuwa katika watu wema.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa Dhun-Nun alipoondoka hali ameghadhibika, na akadhani ya kwamba hatutakuwa na uwezo juu yake. Basi aliita katika giza: Hapana mungu isipo kuwa Wewe Subhanaka Uliye takasika. Hakika mimi nilikuwa miongoni mwa wenye kudhulumu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniBasi tukamwitikia na tukamwokoa kutokana na dhiki. Na hivyo ndivyo tunavyo waokoa Waumini.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa Zakariya alipo mwita Mola wake Mlezi: Mola wangu Mlezi! Usiniache peke yangu, na Wewe ndiye Mbora wa wanao rithi.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniBasi tukamwitikia, na tukampa Yahya na tukamponyeshea mkewe. Hakika wao walikuwa wepesi wa kutenda mema, na wakituomba kwa shauku na khofu. Nao walikuwa wakitunyenyekea.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa mwanamke aliye linda uke wake, na tukampulizia katika roho yetu, na tukamfanya yeye na mwanawe kuwa ni Ishara kwa walimwengu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniKwa hakika huu umma wenu ni umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu Mlezi. Kwa hivyo niabuduni Mimi.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNao wakalikata jambo lao hili mapande mapande baina yao. Wote watarudi kwetu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa atendaye mema naye ni Muumini basi haitakataliwa juhudi yake. Na hakika Sisi tunamwandikia.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa haiwi kwa wana-mji tulio uangamiza, ya kwamba hawatarejea,
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniMpaka watapo funguliwa Juju na Maajuju wakawa wanateremka kutoka kila mlima;
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa miadi ya haki ikakaribia. Hapo ndipo yatapo kodoka macho ya walio kufuru (na watasema:) Ole wetu! Bila ya shaka tulikuwa tumeghafilika na haya, bali tulikuwa wenye kudhulumu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniHakika nyinyi na hao mnao waabudu badala ya Mwenyezi Mungu ni kuni za Jahannamu; huko mtaingia tu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniLau kuwa hawa ni miungu, wasingeli ingia. Na wote watadumu humo.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniLao wao humo ni kupiga mayowe, na wala hawatasikia (jenginelo).
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniAma wale ambao wema wetu umewatangulia, hao watatenganishwa na hayo.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniHawatausikia mvumo wake, na wao watadumu katika yale zinayo yatamani nafsi zao.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniHicho Kitisho Kikubwa hakito wahuzunisha. Na Malaika watawapokea (kwa kuwaambia): Hii ndiyo Siku yenu mliyo kuwa mkiahidiwa!
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniSiku tutakapo zikunja mbingu kama mkunjo wa karatasi za vitabu. Kama tulivyo anza umbo la mwanzo tutalirudisha tena. Ni ahadi iliyo juu yetu. Hakika Sisi ni watendao.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa hakika tulikwisha andika katika Zaburi baada ya Kumbukumbu, ya kwamba nchi watairithi waja wangu walio wema.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniHakika katika haya yapo mawaidha kwa watu wafanyao ibada.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNasi hatukukutuma ila uwe ni Rehema kwa walimwengu wote.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniSema: Hakika imefunuliwa kwangu ya kwamba hakika Mungu wenu ni Mungu Mmoja tu. Je! Mmesilimu?
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa kama wakigeuka, basi sema: Nimekutangazieni sawa sawa, wala sijui yako karibu au mbali hayo mliyo ahidiwa.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniHakika Yeye anajua kauli ya dhaahiri na anajua myafichayo.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniWala sijui pengine huu ni mtihani tu kwenu na starehe mpaka muda kidogo.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniSema: Mola wangu Mlezi! Hukumu kwa haki. Na Mola wetu Mlezi ni Mwingi wa Rehema, aombwaye msaada juu ya mnayo yazua.