الفرقان

Al-Furqan

Sura ya 25 · ya Makka · aya 77 · Mpangilio wa kuteremshwa: 42

Hati
Tafsiri

Gusa neno la Kiarabu ili kuona usomaji, muundo na mzizi wake.

بِسْمِ ٱللَّهِ ٱلرَّحْمَٰنِ ٱلرَّحِيمِ
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniAmetukuka aliye teremsha Furqani kwa mja wake, ili awe mwonyaji kwa walimwengu wote.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniAmbaye ni wake ufalme wa mbingu na ardhi, wala hakuwa na mwana, wala hakuwa na mshirika katika ufalme, na akaumba kila kitu na akakikadiria kwa kipimo.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa wamechukua badala yake miungu ambayo haiumbi chochote, bali hiyo inaumbwa, haijimilikii nafsi zao madhara wala manufaa, wala haimiliki mauti, wala uhai, wala kufufuka.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa wamesema walio kufuru: Haya si chochote ila ni uzushi alio uzua, na wamemsaidia kwa haya watu wengine! Hakika hawa wamekuja na dhulma na uwongo.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa wakasema: Hivi ni visa vya watu wa kale alivyo viandikisha, anavyo somewa asubuhi na jioni.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniSema: Ameyateremsha haya ajuaye siri za katika mbingu na ardhi. Hakika Yeye ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa wakasema: Ana nini Mtume huyu? Anakula chakula, na anatembea masokoni! Mbona hakuteremshiwa Malaika akawa mwonyaji pamoja naye?
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniAu akaangushiwa khazina juu yake, au akawa na bustani ale katika hiyo? Wakasema madhaalimu: Nyinyi hamumfuati ila mtu aliye rogwa.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniTazama jinsi wanavyo kupigia mifano. Basi wamepotea, wala hawataiweza Njia.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniAmetukuka ambaye akitaka atakujaalia yaliyo bora kuliko hayo, nayo ni mabustani yapitayo mito kati yao, na atakujaalia majumba ya fakhari.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniBali wanaikanusha Saa (ya Kiyama). Na Sisi tumemuandalia Moto mkali kabisa huyo mwenye kuikanusha Saa..
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniUle Moto ukiwaona tangu mahali mbali wao watasikia hasira yake na mngurumo wake.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa watakapo tupwa humo mahali dhiki, hali wamefungwa, wataomba wafe.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniMsiombe kufa mara moja tu, bali mfe mara nyingi!
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniSema: Je! Haya ni bora au Pepo ya milele, ambayo wameahidiwa wachamngu, iwe kwao malipo na marejeo?
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniWatayapata humo wayatakayo daima dawamu. Hii ni ahadi juu ya Mola wako Mlezi, inayo ombwa.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa siku atakapo wakusanya wao na hao wanao waabudu, na akasema: Je! Ni nyinyi mlio wapoteza waja wangu hawa, au wao wenyewe walipotea njia?
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniWatasema: Subhanak, Umetakasika na upungufu! Haikutupasia sisi kuchukulia walinzi badala yako, lakini Wewe uliwastarehesha wao na baba zao hata wakasahau kukumbuka, na wakawa watu walio angamia.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniBasi walikukanusheni kwa mliyo yasema. Kwa hivyo hamwezi kujiondolea wala kujisaidia. Na atakaye dhulumu miongoni mwenu tutamwonjesha adhabu kubwa.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa hatukuwatuma kabla yako Mitume wowote ila kwa hakika na yakini walikuwa wakila chakula, na wakenda masokoni. Na tumewajaalia baadhi yenu wawe ni majaribio kwa wengine; je! Mtasubiri? Na Mola wako Mlezi ni Mwenye kuona.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNA WALISEMA wale wasio taraji kukutana nasi: Mbona sisi hatuteremshiwi Malaika au hatumwoni Mola wetu Mlezi? Kwa yakini hawa wamejiona bora nafsi zao, na wamepanda kichwa vikubwa mno!
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniSiku watakayo waona Malaika haitakuwa furaha siku hiyo kwa wakosefu. Na watasema: Mungu apishe mbali!
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa tutayaendea yale waliyo yatenda katika vitendo vyao, tuvifanye kama mavumbi yaliyo tawanyika.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniWatu wa Peponi siku hiyo watakuwa katika makaazi bora na mahali penye starehe nzuri.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa siku zitapo funguka mbingu kwa mawingu, na wateremshwe Malaika kwa wingi,
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniUfalme wa haki siku hiyo utakuwa wa Arrahman, Mwingi wa Rehema, na itakuwa siku ngumu kwa makafiri.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa siku ambayo mwenye kudhulumu atajiuma mikono yake, na huku anasema: Laiti ningeli shika njia pamoja na Mtume!
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniEe Ole wangu! Laiti nisingeli mfanya fulani kuwa rafiki!
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniAmenipoteza, nikaacha Ukumbusho, baada ya kwisha nijia, na kweli Shet'ani ni khaini kwa mwanaadamu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa Mtume alikuwa akisema: Ee Mola wangu Mlezi! Hakika watu wangu wameifanya hii Qur'ani ni kihame.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa vivi hivi tumemfanyia kila Nabii adui miongoni mwa wakosefu, na Mola wako Mlezi anatosha kuwa Mwenye kuongoa na Mwenye kunusuru.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa wakasema walio kufuru: Kwa nini hakuteremshiwa Qur'ani kwa jumla moja? Hayo ni hivyo ili tuuthibitishe moyo wako, na ndio tumeisoma kwa mafungu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniWala hawatakuletea mfano wowote, ila na Sisi tutakuletea (jawabu) kwa haki, na tafsiri iliyo bora.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniWale ambao watakao kusanywa na kubururwa kifudifudi mpaka kwenye Jahannamu, hao watakuwa na mahali pabaya, ndio wenye kuipotea sana njia.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa hakika tulimpa Musa Kitabu na tukamweka pamoja naye nduguye, Harun, kuwa waziri.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniTukawaambia: Nendeni kwa watu walio kanusha Ishara zetu. Basi tukawateketeza kabisa.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa watu wa Nuhu, walipo wakanusha Mitume, tuliwazamisha, na tukawafanya ni Ishara kwa watu. Na tumewaandalia wenye kudhulumu adhabu chungu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa tuliwaangamiza kina A'di na Thamudi na watu wa Rass na vizazi vingi vilivyo kuwa kati yao.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa wote tuliwapigia mifano, na wote tuliwaangamiza kabisa kabisa.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa kwa yakini wao wanafika kwenye nchi ilio teremshiwa mvua mbaya. Basi, je, hawakuwa wakiiona? Bali walikuwa hawataraji kufufuliwa.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa wanapo kuona hawakuchukulii ila ni mzaha tu, na (wanasema): Ati ndiye huyu Mwenyezi Mungu aliye mtuma kuwa Mtume?
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniKwa hakika alikuwa karibu kutupoteza tuiache miungu yetu, ingeli kuwa hatukushikamana nayo kwa kuvumilia. Bado watakuja jua, watakapo iona adhabu, ni nani aliye potea njia.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniJe! Umemwona aliye yafanya matamanio yake kuwa ndio mungu wake? Basi je, wewe utakuwa ni wakili wake?
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniAu wewe unadhani kwamba wengi wao wanasikia au wanaelewa? Hao hawakuwa ila ni kama nyama hoa tu, bali wao wamepotea zaidi njia.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniJe! Huoni jinsi Mola wako Mlezi anavyo kitandaza kivuli. Na angeli taka angeli kifanya kikatulia tu. Kisha tumelifanya jua kuwa ni kiongozi wake.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniKisha tunakivutia kwetu kidogo kidogo.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNaye ndiye aliye kufanyieni usiku kuwa ni vazi, na usingizi kuwa mapumziko, na akakufanyieni mchana ni kufufuka.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNaye ndiye anaye zituma pepo kuwa bishara njema kabla ya rehema yake, na tunayateremsha kutoka mbinguni maji safi.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniIli kwa hayo tuihuishe nchi iliyo kufa, na tuwanyweshe wanyama na watu wengi tulio waumba.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa kwa yakini tumeisarifu kati yao wapate kukumbuka. Lakini watu wengi wanakataa ila kukufuru.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa tungeli taka tungeli peleka katika kila mji Mwonyaji.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniBasi usiwat'ii makafiri. Na pambana nao kwayo kwa Jihadi kubwa.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNaye ndiye aliye zipeleka bahari mbili, hii tamu mno, na hii ya chumvi chungu. Na akaweka baina yao kinga na kizuizi kizuiacho.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNaye ndiye aliye muumba mwanaadamu kutokana na maji, akamjaalia kuwa na nasaba na ushemeji. Na Mola wako Mlezi ni Muweza.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa wanayaabudu badala ya Mwenyezi Mungu yasiyo wafaa wala yasiyo wadhuru. Na kafiri daima ni msaidizi wa kumpinga Mola wake Mlezi.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNasi hatukukutuma ila kuwa ni Mbashiri na Mwonyaji.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniSema: Sikukuombeni ujira juu yake; ila atakaye na ashike njia iendayo kwa Mola wake Mlezi.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa mtegemee Aliye Hai, ambaye hafi. Na umtukuze kwa sifa zake. Na yatosha kwake kuwa yeye ni Mwenye khabari za dhambi za waja wake.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniAmbaye ameziumba mbingu na ardhi, na viliomo ndani yake kwa siku sita. Kisha akatawala juu ya A'rshi, Arrahman, Mwingi wa Rehema! Uliza khabari zake kwa wamjuaye.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa wanapo ambiwa: Msujudieni Arrahman! Wao husema: Ni nani Arrahman? Je! Tumsujudie unaye tuamrisha wewe tu? Na huwazidishia chuki.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniAmetukuka aliye zijaalia nyota mbinguni, na akajaalia humo taa na mwezi unao ng'ara.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNaye ndiye aliye fanya usiku na mchana kufuatana kwa nafuu ya anaye taka kukumbuka, au anaye taka kushukuru.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa waja wa Arrahman Mwingi wa Rehema ni wale wanao tembea ulimwenguni kwa staha, na wajinga wakiwasemeza hujibu: Salama!
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa wale wanao kesha kwa ajili ya Mola wao Mlezi kwa kusujudu na kusimama.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa wale wanao sema: Mola wetu Mlezi! Tuondolee adhabu ya Jahannamu. Hakika adhabu yake ikimpata mtu haimwachi.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniHakika hiyo ni kituo na makao mabaya.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa wale ambao wanapo tumia hawatumii kwa fujo wala hawafanyi ubakhili, bali wanakuwa katikati baina ya hayo.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa wale wasio mwomba mungu mwengine pamoja na Mwenyezi Mungu, wala hawaui nafsi aliyo iharimisha Mwenyezi Mungu isipo kuwa kwa haki, wala hawazini - na atakaye fanya hayo atapata madhara,
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniAtazidishiwa adhabu Siku ya Kiyama, na atadumu humo kwa kufedheheka.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniIsipo kuwa atakaye tubu, na akaamini, na akatenda vitendo vyema. Basi hao Mwenyezi Mungu atayabadilisha maovu yao yawe mema. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa aliye tubu na akafanya mema, basi hakika huyo ametubu kweli kweli kwa Mwenyezi Mungu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa wale ambao hawatoi ushahidi wa uwongo, na pindi wapitapo penye upuuzi, hupita kwa hishima yao.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa wale ambao wanapo kumbushwa Ishara za Mola wao Mlezi hawajifanyi viziwi nazo, na vipofu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa wale wanao sema: Mola wetu Mlezi! Tupe katika wake zetu na wenetu yaburudishayo macho, na utujaalie tuwe waongozi kwa wachamngu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniHao ndio watakao lipwa makao ya juu kwa kuwa walisubiri, na watakuta humo maamkio na salamu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniWadumu humo - kituo na makao mazuri kabisa.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniSema: Mola wangu Mlezi asinge kujalini lau kuwa si kuomba kwenu. Lakini nyinyi mmemkadhibisha. Basi adhabu lazima iwe.