يس

Ya-Sin

Sura ya 36 · ya Makka · aya 83 · Mpangilio wa kuteremshwa: 41

Hati
Tafsiri

Gusa neno la Kiarabu ili kuona usomaji, muundo na mzizi wake.

بِسْمِ ٱللَّهِ ٱلرَّحْمَٰنِ ٱلرَّحِيمِ
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniYa-Sin (Y. S.).
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniKwa Haki ya Qur'ani yenye hikima!
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniHakika wewe ni miongoni mwa walio tumwa,
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniJuu ya Njia Iliyo Nyooka.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniUteremsho wa Mwenye nguvu, Mwenye kurehemu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniIli uwaonye watu ambao baba zao hawakuonywa, basi wao wamekuwa wenye kughafilika.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniBila ya shaka kauli imekwisha thibiti juu ya wengi katika wao, kwa hivyo hawaamini.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniTumeweka makongwa shingoni mwao, yakawafika videvuni. Kwa hivyo vichwa vyao viko juu tu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniTumeweka kizuizi mbele yao, na kizuizi nyuma yao, na tumewafunika macho yao; kwa hivyo hawaoni.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNi sawa sawa kwao ukiwaonya au usiwaonye, hawataamini.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniHakika wewe unamwonya mwenye kufuata ukumbusho, na akamcha Arrahman, Mwingi wa Rehema, kwa ghaibu. Basi mbashirie huyo msamaha na ujira mwema.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniHakika Sisi tunawafufua wafu, na tunayaandika wanayo yatanguliza, na wanayo yaacha nyuma. Na kila kitu tumekihifadhi katika daftari asli lenye kubainisha.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa wapigie mfano wa wakaazi wa mji walipo wafikia walio tumwa.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniTulipo watumia wawili, wakawakanusha. Basi tukawazidishia nguvu kwa mwingine wa tatu. Wakasema: Hakika sisi tumetumwa kwenu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniWakasema: Nyinyi si chochote ila ni watu kama sisi. Na Mwingi wa Rehema hakuteremsha kitu. Nyinyi mnasema uwongo tu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniWakasema: Mola wetu Mlezi anajua kwamba hakika sisi tumetumwa kwenu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniWala si juu yetu ila kufikisha ujumbe ulio wazi.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniWakasema: Sisi tumeagua kuwa nyinyi ni wakorofi. Ikiwa hamtaacha basi kwa yakini tutakupigeni mawe, na mtapata adhabu chungu kutoka kwetu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniWakasema: Ukorofi wenu mnao wenyewe! Je! Ni kwa kuwa mnakumbushwa? Ama nyinyi ni watu walio pindukia mipaka.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa akaja mtu mbio kutokea upande wa mbali wa mjini, akasema: Enyi watu wangu! Wafuateni hawa walio tumwa.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniWafuateni ambao hawakutakini ujira, hali ya kuwa wenyewe wameongoka.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNA KWA NINI nisimuabudu yule aliye niumba na kwake mtarejeshwa?
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniJe! Niishike miungu mingine badala yake? Arrahmani, Mwingi wa Rehema, akinitakia madhara uombezi wa hao hautanifaa kitu, wala hawataniokoa.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniBasi hakika mimi hapo nitakuwa katika upotovu ulio dhaahiri.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniHakika mimi nimemuamini Mola wenu Mlezi, basi nisikilizeni!
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniAkaambiwa: Ingia Peponi! Akasema: Laiti kuwa watu wangu wangeli jua
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniJinsi Mola wangu Mlezi alivyo nisamehe, na akanifanya miongoni mwa walio hishimiwa.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa hatukuwateremshia kaumu yake baada yake jeshi kutoka mbinguni, wala si wenye kuteremsha.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniHakukuwa ila ukelele mmoja tu; na mara walizimwa!
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNawasikitikia waja wangu. Hawajii Mtume ila wao humkejeli.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniJe! Hawaoni umma ngapi tulizo ziangamiza kabla yao? Hakika hao hawarejei tena kwao.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa hapana mmoja ila wote watakusanywa waletwe mbele yetu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa Ishara hiyo kwao - ardhi iliyo kufa, nasi tukaifufua, na tukatoa ndani yake nafaka, wakawa wanazila!
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa tukafanya ndani yake mabustani ya mitende na mizabibu, na tukatimbua chemchem ndani yake,
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniIli wale matunda yake, na hayo hayakufanywa na mikono yao! Basi je, hawashukuru?
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniSubhana, Ametakasika, aliye umba dume na jike vyote katika vinavyo mea katika ardhi na katika nafsi zao, na katika wasivyo vijua.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa usiku ni Ishara kwao. Tunauvua humo mchana, mara wao wanakuwa gizani.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa jua linakwenda kwa kiwango chake. Hayo ni makadirio ya Mwenye nguvu, Mwenye kujua.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa mwezi tumeupimia vituo, mpaka unakuwa kama karara kongwe.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniHaliwi jua kuufikia mwezi, wala usiku kuupita mchana. Na vyote vinaogelea katika njia zao.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa ni Ishara kwao kwamba Sisi tuliwapakia dhuriya zao katika jahazi ilio sheheni.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa tukawaumbia kutoka mfano wake wanavyo vipanda.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa tukitaka tunawazamisha, wala hapana wa kuwasaidia, wala hawaokolewi,
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniIsipo kuwa kwa rehema zitokazo kwetu na starehe kwa muda.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa wanapo ambiwa: Jilindeni na yalioko mbele yenu na yalioko nyuma yenu, ili mpate kurehemewa...
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa haiwafikii Ishara yoyote katika Ishara za Mola wao Mlezi ila wao huwa ni wenye kuipuuza.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa wanapo ambiwa: Toeni katika aliyo kupeni Mwenyezi Mungu, walio kufuru huwaambia walio amini: Je! Tuwalishe ambao Mwenyezi Mungu angependa angeli walisha mwenyewe? Nyinyi hammo ila katika upotofu ulio dhaahiri.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa wanasema: Ahadi hii itatokea lini, ikiwa nyinyi ni wakweli?
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniHawangojei ila ukelele mmoja tu utakao wachukua nao wamo kuzozana.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniBasi hawataweza kuusia, wala kwa watu wao hawarejei.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa litapulizwa barugumu, mara watatoka makaburini wakikimbilia kwa Mola wao Mlezi.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniWatasema: Ole wetu! Nani aliye tufufua kwenye malazi yetu? Haya ndiyo aliyo yaahidi Mwingi wa Rehema na wakasema kweli Mitume.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniHaitakuwa ila ukelele mmoja tu, mara wote watahudhuruishwa mbele yetu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniBasi leo nafsi yoyote haitadhulumiwa kitu, wala hamtalipwa ila yale mliyo kuwa mkiyatenda.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniHakika watu wa Peponi leo wamo shughulini, wamefurahi.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniWao na wake zao wamo katika vivuli wameegemea juu ya viti vya fakhari.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniWatapata humo kila namna ya matunda na watapata kila watakacho kitaka.
  1. Ali Muhsin Al-Barwani"Salama!" Hiyo ndiyo kauli itokayo kwa Mola Mlezi Mwenye kurehemu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa enyi wakosefu! Jitengeni leo!
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniJe! Sikuagana nanyi, enyi wanaadamu, kuwa msimuabudu Shet'ani? Hakika yeye ni adui dhaahiri kwenu.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa ya kwamba mniabudu Mimi? Hii ndiyo Njia Iliyo Nyooka.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa bila ya shaka yeye amekwisha lipoteza kundi kubwa miongoni mwenu. Je, hamkuwa mkifikiri?
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniHii basi ndiyo Jahannamu mliyo kuwa mkiahidiwa.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniIngieni leo kwa vile mlivyo kuwa mkikufuru.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniLeo tunaviziba vinywa vyao, na iseme nasi mikono yao, na itoe ushahidi miguu yao kwa waliyo kuwa wakiyachuma.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa tungeli penda tungeli yafutilia mbali macho yao, wakawa wanaiwania njia. Lakini wange ionaje?
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa tungeli taka tunge wageuza sura hapo hapo walipo, basi wasinge weza kwenda wala kurudi.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa tunaye mzeesha tunamrudisha nyuma katika umbo. Basi je! hawazingatii?
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniWala hatukumfundisha (Muhammad) mashairi, wala hayatakikani kwake hayo. Haukuwa huu ila ni ukumbusho na Qur'ani inayo bainisha.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniIli imwonye aliye hai, na neno litimie juu ya makafiri.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniJe! Hawaoni kwamba tumewaumbia kutokana na iliyo fanya mikono yetu wanyama wa mifugo, na wao wakawa wenye kuwamiliki.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa Sisi tukawadhalilishia. Basi baadhi yao wako wanao wapanda, na baadhi yao wanawala.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa wao wanapata kwao manufaa na vinywaji. Basi je, hawashukuru?
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa wameishika miungu mingine badala ya Mwenyezi Mungu ili ati wapate kusaidiwa!
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniHawataweza kuwasaidia. Bali hao ndio watakuwa askari wao watakao hudhurishwa.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniBasi maneno yao yasikuhuzunishe. Hakika Sisi tunayajua wanayo yaweka siri na wanayo yatangaza.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniKwani mwanaadamu haoni ya kwamba Sisi tumemuumba yeye kutokana na tone la manii? Kisha sasa yeye ndio amekuwa ndiye mgomvi wa dhaahiri!
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniNa akatupigia mfano, na akasahau kuumbwa kwake, akasema: Ni nani huyo atakaye ihuisha mifupa nayo imekwisha mung'unyika?
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniSema: Ataihuisha huyo huyo aliye iumba hapo mara ya mwanzo. Na Yeye ni Mjuzi wa kila kuumba.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniAliye kujaalieni kupata moto kutokana na mti wa kijani nanyi mkawa kwa huo mnawasha.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniKwani aliye ziumba mbingu na ardhi hawezi kuwaumba mfano wao? Kwani! Naye ndiye Muumbaji Mkuu, Mjuzi.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniHakika amri yake anapo taka kitu ni kukiambia tu: Kuwa! Na kikawa.
  1. Ali Muhsin Al-BarwaniBasi Ametakasika yule ambaye mkononi mwake umo Ufalme wa kila kitu; na kwake Yeye mtarejeshwa.